Ali Said Mbwana maarufu kama Bushiri Mpemba alikuwa ni muigizaji wa tamthilia na mwandishi
aliyepata umaarufu mkubwa miaka ya tisini mwishoni na elfu mbili mwanzoni. Lafudhi yake ya kipemba
na msemo wake maarufu wa Yakhe mbona mwanzingua nyie? Taarabu imo humo? Ndio ilikuwa
kitambulisho chake kikubwa katika ulimwengu wa maigizo. Muigizaji huyu aliyebobea kwenye kuigiza na
kuandika ni mzaliwa wa Arusha, aliyezaliwa tarehe 23, Agosti mwaka 1951.
Mwaka 1998 akishirikiana na wenzake walianzisha kundi la kisanaa lijilikanalo kama “Tausi Theater
Ensemble” na Ali Mbwana akisimama kama katibu, huku wakifanikiwa kucheza maigizo na kuanza
kurushwa rasmi kwenye runinga ikiwemo ITV. Licha ya kufanya maigizo walifanikiwa kucheza filamu ya
“Tubadilike” ambayo ilishirikisha pia baadhi ya walimu wa chuo cha sanaa Bagamo. Huku Ali Mbwana
akiwa na malengo yakuja kuwa mwandishi mzuri sana wa hadithi.
Chimbuko la Sanaa yake ni kutoka kwenye familia yao ambayo imejihusisha na Sanaa kwa muda mrefu.
Ali Mbwana angali akiwa kijana mdogo huko Tanzania visiwani alipenda sana kujihusisha na Sanaa.
Mwaka 1977 alifanikiwa kufanya kazi katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kama msaidizi wa
maktaba, na ndipo safari yake ya kujihusisha na sanaa ya uigizaji ilipoanza na kushamiri katika chuo
hicho. Na mwaka 1981 alifanikiwa kujiunga rasmi katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam kama
mwanafunzi wa masomo ya sanaa, ambapo alichukua kozi ya Shahada katika sanaa na ukumbi wa
michezo (Bachelor in fine arts and theatre).
Akiwa bado ni mwanafunzi, kwa mara ya kwanza mwaka 1982 alianza kujihusisha na kuonekana kwenye
maigizo ya jukwaani akiwa chini ya kikundi cha “Paukwa Theatre Esemble’’, na mwaka 1984 baada ya
kuhitimu shahada yake ya kwanza akawa mwanachama rasmi wa kikundi hicho, huku akitaja jukwaa
ndiyo sehemu pekee alipoanza rasmi sanaa yake na kujijenga katika misingi ya kisanaa.
Akiwa katika kikundi cha “Paukwa Theatre Esemble” walipata mafanikio makubwa na kufanikiwa
kwenda kushiriki michezo ya jukwaani kwenye nchi za ughaibuni kama Sweden na Denmark. Lakini pia
kabla ya kuhitimu masomo yake katika Chuo kikuu cha Dar es salaam, alianza kushiriki taratibu kuigiza
katika michezo ya redioni kama vile “Baba kidawa” na baadae akashiriki kwenye mchezo mwengine wa
“Twende na wakati” iliyorushwa kwenye Redio Tanzania, huku ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki
kwenye michezo ya redio.
Licha ya kujihusisha na uigizaji pia alianza kuhusika kwenye uandishi wa hadithi za michezo, hii ni baada
ya kufanikiwa kupata nafasi ya kuteuliwa kusoma kozi fupi ya uandishi na baadae akawa mmoja wa
waandishi rasmi katika mchezo wa “Twende kwa wakati”. Ndipo baadae Redio Tanzania ikaingia
makubaliano na Media for Development International (MFD), kwenye suala zima la kurusha michezo
kwenye redio. Ali Mbwana alifanikiwa kuteuliwa kufanya kazi kama mwandishi mkuu wa michezo ya
redio iliyochini ya MFDI, na mchezo wa kwanza kufanyika ulijulikana kama “Wahapa hapa” na Ali
Mbwana akiwa kama mwandishi mkuu. Mchezo mwengine uliitwa ‘’Chuma” na aliweza kushiriki moja
kwa moja kutafsiri mchezo huo, badae pia alishiriki kwenye kuandika tamthilia ya “Siri ya Mtungi”.
Mbali na kuandika michezo ashiriki pia kwenye uandishi wa matangazo kadha wa kadha ikiwemo,
tangazo la “Fataki’’ chini ya MFDI ambalo alisimama kama mwandishi mkuu likihusisha msani mkubwa
Tanzania, Mrisho Mpoto nakujichukulia hadhira wengi sana walilo lipenda tangazo hilo.